Alhamisi , 25th Feb , 2016

Kocha mkuu wa klabu ya soka ya Azam Fc Muingereza Stewart Hall ametupa lawama kwa waamuzi wa mechi yao ya jana ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Tanzania Prisons kuwa ndiye aliyepelekea wao kushindwa kuibuka na alama tatu muhimu.

Kocha mkuu wa Azam Fc Stewart Hall

Akizungumza mara baada ya mechi kumalizika Hall amesema mwamuzi alishindwa kumudu mchezo huku akionekana kuwapendelea wenyeji wa mechi hiyo waliokuwa wakicheza kibabe badala ya kucheza mpira.

Muingereza huyo amekiri kuwa mechi ilikuwa ngumu lakini mwamuzi ndiye alichangia kuruhusu hali hiyo kwa kuwa siku zote refa ndiye mwenye uwezo wa kufanya mechi kuwa katika mazingira kama hayo.

Kwa upande wake kocha wa Tanzania Prisons Salum Mayanga amesema watafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza jana huku akimjibu kocha wa Azam kuwa wao hawajabebwa kama anavyofikiria.

Mayanga amemtaka kocha wa Azam kufanyia kazi changamoto alizokutana nazo ili aweze kukabiliana nazo hasa katika medali za kimataifa ikiwa wao ndio wawakilishi wa Tanzania katika kombe la shirikisho barani Afrika.