
Kocha mpya wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer
Meneja huyo wa Cardiff City Neil Warnock amesema kuwa Ole Gunnar Solskjaer ana nafasi kubwa ya kufanya kazi kwa mkataba mrefu na Manchester United baada ya kuchukua nafasi ya Jose Mourinho kuwa kocha wa muda mfupi klabuni hapo.
Akizungumzia juu ya uteuzi wa kocha huyo mpya wa Man United na namna ambavyo atadumu klabuni hapo, Neil Warnock amesema, "bila shaka kabisa, anaweza kupewa mkataba mrefu zaidi endapo atafanya vizuri katika miezi yake sita aliyopewa".
"Ana wachezaji wazuri, itakuwa ni siku kubwa na ya furaha kuona anaingia katika chumba cha kubadilisha nguo hapo kesho. Yeye ni shujaa pale, ni mchezaji mkubwa mwenye historia, ataunyanyua mlima," amesema.
Solskjaer ataanza kampeni yake ya ligi akiwa kocha mpya wa Manchester United dhidi ya Cardiff City wikiendi hii ugenini katika dimba la Cardiff.
Jose Mourinho alifukuzwa Jumanne, siku mbili baada ya kufungwa mabao 3-1 dhidi ya mpinzani wake wa mafanikio katika EPL, Liverpool, na kuachwa kwa tofauti ya pointi 19 pointi katika msimamo wa ligi hiyo.
Ingawa inaripotiwa kuwa uamuzi wa Man United kumwajiri Solskjaer kuwa Meneja wa muda mfupi ni kutokana na lengo lake la kutaka kumsajili kocha wa Tottenham Hortspurs, Mauricio Pochettino, Warnock anadhani kuwa Solskjaer ana nafasi ya kocha wa kudumu klabuni hapo.