''Kuna watu walianza kuomba Taifa Stars ifungwe''

Alhamisi , 4th Jul , 2019

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, amewataka watanzania kuacha makundi na kuwa pamoja kwenye nyakati zote hususani mambo ya kitaifa, kama ushindi wa Taifa Stars ambao sio wa Makonda peke yake.

Paul Makonda akiwa na kocha wa Taifa Stars Emmanuel Amunike.

Makonda ameyasema hayo kwenye mapokezi ya Taifa Stars kwenye uwanja wa ndege wa JK Nyerere, ambapo ameeleza kuwa timu hiyo inahitaji pongezi na kujipanga kwaajili ya michuano mingine kama CHAN.

''Ilifika wakati watu wakawa wanaona kama hii ni timu ya Makonda na kuomba pengine ifungwe, lakini ikishinda inakuwa ni timu ya taifa, naomba tuache hiyo tabia tuwe tunaitumia taifa Stars kuwa wamoja na kuwajenga wachezaji wetu'', amesema.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa anazo taarifa amezibaini kule nchini Misri kuwa kuna taasisi ilichangisha fedha kwaajili ya Taifa Stars lakini haikuziwakilisha na badala yake wao wakazitumia kwenda kufanya starehe Misri.

''Wanajijua niwaombe tu kama ambavyo akaunti imetangazwa na Waziri wa Michezo wazifikishe huko au wazipeleke Baraza la Michezo (BMT), haiwezekani wachezaji hawapati morali kwa posho nzuri, hatutaelewana kwakweli'', ameongeza.