Jumanne , 3rd Mei , 2016

Leicester City watajizolea Dola milioni 200 baada ya kufanikiwa kushinda Ligi Kuu ya Uingereza.

Pesa hizo zinatokana na tuzo ya kushinda Ligi ya Premia, pesa za kushiriki Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, na ongezeko la mapato ya kila siku kutokana na mauzo ya tiketi.

Klabu hiyo pia itajivunia kupanda kwa thamani ya udhamini na pia ongezeko la mashabiki duniani.

Hata hivyo Klabu hiyo ya Leicester City itashiriki katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao jambo litakalowawezesha kutazamwa na watu wengi zaidi kwenye runinga Ulaya na kote duniani.

Afisa mkuu wa ushauri wa kitaalamu wa Uingereza anasema kwamba mashabiki huwa na umuhimu mkubwa kwa klabu na watachangia sana katika ukuaji wa Leicester kibiashara.

Msimu huu, wafuasi wa Leicester City katika Facebook waliongezeka 540%, ongezeko kubwa zaidi miongoni mwa klabu za michezo duniani.

Nchini Algeria klabu hiyo ina wafuasi 500,000 kwenye Facebook na kumeshuhudiwa pia ongezeko kubwa la mashabiki Thailand na Italia.

Mmiliki wa klabu hiyo Vichai Srivaddhanaprabha ni raia wa Thailand naye meneja Claudio Ranieri ni Mwitaliano.