Jumanne , 21st Jun , 2016

Chama cha ngumi mkoa wa Dar es Salaam DABA kimeandaa mashindano maalumu ya klabu bingwa ya mkoa huo kwa mara ya kwanza yenye hadhi ya kimataifa huku yakishirikisha mabondia kutoka vilabu mbalimbali katika nchi za Kenya, Nigeria na wenyeji Tanzania

Mabondia wakichuana katika moja ya mashindano ya mkoa wa Dar es Salaam.

Zaidi ya mabondia 100 kutoka vilabu mbalimbali hapa nchini na nchi alikwa aza Kenya na Nigeria wanataraji kushiriki michuano ya kimataifa ya klabu bingwa ya mkoa wa Dar es Salaam ambayo itaanza kesho jioni katika uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa zoezi la upimaji uzito wa mabondia hao Mwenyekiti wa chama cha ngumi mkoa wa Dar es Salaam DABA Akalori Godfrey amesema mabondia hao watachuana katika uzito mwepesi hadi hadi wa juu.

Aidha Akalori amesema vilabu vyote shiriki na mabondia wao wameshapimwa afya zao na uzito na wanataraji mashindano hayo yatawasaidia kupata kikosi bora cha mkoa na pia yatatumika kuwasaidia viongozi wa kamati ya ufundi ya shirikisho la ngumi taifa BFT kuangalia uwezo wa mabondia wapya ama wale waliopo katika timu ya taifa ya sasa ili kuwapa nafasi ya kwenda kushiriki mashindano ya mchujo kuwania tiketi ya kushiriki michuano ya Olimpiki ya Rio Brazil ambayo yatafanyika nchini Venezuela mapema mwezi Julai mwaka huu.

Nao wawakilishi wa timu alikwa za Nigeria na Kenya wanazungumzia ushiriki wao katika michuano hiyo ambapo mwakilishi wa Nigeria anasema pamoja na kushindana lakini wamekuja nchini kwajli ya kutoa uzoefu wao na kukuza mchezo huo.

Kwa upande wake Adesoji Babalola ambaye ni mwakilishi wa timu ya Nigeria amesema wamekubali mwaliko huo hasa ikizingatiwa kuwa wanataka kupata changamoto mpya kutoka kwa wapiganaji wa Tanzania lakini kubwa ni kuwapa uzoefu mabondia wetu na mbinu mbalimbali za mchezo huo kutokana na uzoefu wao wa kushiriki michuano mbalimbali barani Afrika, Asia na America wakicheza katika nchi za Thailand, China na Brazil.

Aidha Adesoji ambaye pia ni kocha amesema kubwa lingine ni kutoa mafunzo kwa viongozi wa mchezo huo mkoa wa Dar es Salaam katika masuala ya menejimenti na utawala wa mambo mbalimbali ya mchezo huo kwa levo ama kiwango cha kimataifa kama wanavyojiendesha wao kupitia chama cha ngumi nchini humo [NBA].

Naye Musa Benjamin mwakilishi wa vilabu viwili shiriki kutoka nchini Kenya vya Mombasa na Nairobi amesema watatumia michuano hiyo kama maandalizi ya mabondia hao ambao wamechaguliwa hivi karibuni kujaribu kurekebisha mapungufu yao kabla ya kwenda kwenye michuano ya dunia kwa vijana na ndiyo maana hata vikosi vya timu hizo vinaundwa na mabondia chipukizi ambao wametoka kuteuliwa katika michuano ya taifa iliyofanyika nchini kwao hivi karibuni.