Jumatano , 30th Aug , 2017

Ikiwa zimebakia siku mbili vumbi kutimka katika michuano ya Sprite BBall Kings hatua ya mwisho ya fainali, manahodha wa timu shiriki wameanza kutunishiana misuli kwa kila mmoja kujivutia kwake kuwa atakinyakuwa kikombe cha mashindano hayo.

Akizungumza nahodha wa timu ya TMT, Isihaka Masoud amesema wamejifua vizuri katika kuelekea mechi hiyo huku akidai 'game' hiyo itakuwa yenye ushindani mkubwa kwa kuwa kila mmoja amejipanga kupata matokeo yaliyokuwa mazuri.

"Nina imani mechi ijayo (game 5) ya fainali za Sprite BBall Kings itakuwa nzuri kwa sababu timu yetu imejiandaa vizuri. Safari hii tutakuja tofauti kwa kuwa tunapitia 'step' zote tulizozipitia katika michuano hii",alisema Masoud.

Kwa upande wake nahodha wa Mchenga BBall Stars, Mohamed Yusuph 'Muddy' amesema timu yake imejiandaa vizuri katika kupambana na wapinzani wao huku akijitapa kwa kuwataka mashabiki zao wajitokeze kwa wingi kushuhudia wanavyo kibeba kikombe chao.

"TMT wamechelewesha ubingwa tu ila sisi nafasi yetu iko pale pale katika kukinyakua kikombe. Tunawalika mashabiki wetu wote waje kwa wingi kushuhudia 'basketball inavyochezwa na Mchenga kwa kuwa tumejipanga kuchukua ubingwa asubuhi kweupee", alisema Muddy.

Mchenga BBall Stars na TMT wanakutana tena kwa mara ya mwisho Septemba 2 mwaka huu katika mechi ya mwisho ya fainali za Sprite BBall Kings 'game 5' zitazopigwa katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambapo mechi hiyo ndiyo itakayoweza kumtambulisha mshindi rasmi wa michuano ya Sprite BBall Kings kwa mwaka 2017.