Jumatatu , 25th Jan , 2021

Mataifa ya Mali na Cameroon yamekuwa ya kwanza kukata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya CHAN, baada ya kumaliza katika nafasi za juu kundi A.

hili ndilo kombe la CHAN linalowaniwa na timu 16 katika mashindano ya mwaka huu

Mali wamemaliza vinara wa kundi hilo kwa alama 7, mara baada ya kupata ushindi katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo dhidi ya Zimbabwe inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba Zdravko Logarusic.

Cameroon wao wamemaliza katika nafasi ya pili katika kundi hilo, wakiwa na alama 5 baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Burkina Faso, katika mchezo wa mwisho, uliokuwa na vuta ni kuvute kuwania nafasi hiyo muhimu iliyokuwa wazi kwa yeyote kufuzu.

Hadi sasa ni mataifa hayo mawili tu, ndiyo yaliyofuzu katika hatua hiyo ya robo fainali huku wakisubiri wapinzani wao kutoka kundi B, ambapo mechi zake zinachezwa leo jumatatu ya tarehe 25/01/2021 kati ya Congo Brazzaville dhidi ya Libya na ule wa Niger vs DR Congo.

Kinara wa kundi B atamfuata Cameroon aliyeshika nafasi ya pili katika kundi A, huku mshindi wa pili wa kundi B akimfuata Mali aliyeongoza kundi hilo. Michezo ya robo fainali itaanza kupigwa tarehe 30/1/2021.

Tanzania tutamaliza mchezo wetu wa mwisho tarehe 27/1/2021 vs Guinea na kujua hatma yetu, kama tunasonga mbele katika hatua ya robo fainali au hatusongi, mazingira ya kundi letu yanatuweka katika eneo moja tu la ushindi tu ili tuweze kufuzu.