Manara amshtaki Zahera, avujisha siri yake

Ijumaa , 15th Mar , 2019

Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema anazo taarifa za uhakika kuwa kocha wa Yanga Mwinyi Zahera, hajaondoka nchini badala yake anafanya kazi na AS Vita kinyume na kibali alichopewa na serikali.

Haji Manara na Mwinyi Zahera

Akiongea leo kwenye Kipenga Xtra ya East Africa Radio, Manara amesema Zahera aliaga kuwa anakwenda DR Congo lakini yupo hapa Dar es salaam anafanya kazi na AS Vita na hilo wanalijua.

''Niseme tu kwamba Zahera tunajua habari zake, hajasafiri na timu yake ya Yanga kwenda Iringa na wala hajaenda DR Congo kama alivyoaga, namwambia tu kuwa asisahau kibali chake cha kazi hapa ni kufanyakazi na Yanga sio AS Vita kwahiyo mamlaka zinajua na atajikuta matatani'', - Manara.

Kwa upande mwingine Manara amesema Simba imejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa klabu bingwa Afrika dhidi ya AS Vita kesho Jumamosi saa 1:00 jioni kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam.

Simba ipo nafasi ya mwisho kwenye Kundi D lakini ina nafasi ya kufuzu endapo itashinda mchezo wa kesho dhidi ya AS Vita huku Al Ahly na JS Saoura ambao watacheza Misri nao kutoa timu moja itakayofuzu endapo mmoja atashinda au kutoa sare.