
Haji Manara akiwa na kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera (katikati) na kocha wa Simba, Patrick Aussems (kulia)
Manara amesema kuwa Aussems anajua mchango wa wachezaji na mashabiki katika mafanikio ya timu na ndiyo maana hajawahi kuwazungumzia vibaya wachezaji wake katika mikutano mbalimbali na wanahabari.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Manara ameandika, "huyu kocha ana heshima sana, habwabwaji hovyo na anajua thamani ya wachezaji wake, sijawahi kumsikia akiwaponda hadharani hata siku moja. Ukimsikiliza hapo ombi lake kwa wanahabari utajua kwa nini tunamwita 'Professor', anajua nguvu ya mashabiki kwenye soka!! . Ni Kufa au kupona".
Kauli hiyo ya Manara inakuja baada ya kocha wa watani wao wa jadi Yanga, Mwinyi Zahera kuonekana katika mikutano mbalimbali ya wanahabari akiwakosoa wachezaji wake hadharani tangu alipojiunga na klabu hiyo.
Moja ya kauli ambayo kocha huyo wa Yanga aliwahi kuitoa kwa wachezaji wake Novemba 23 alipokuwa akimzungumzia mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Ajib , baada ya kumsimamisha kutocheza mechi kufuatia kutohudhuria mazoezi.
Zahera alisema, "wakati mimi nasafiri kwenda kwenye timu ya taifa nchini Congo, nilimuachia kocha programu ya mazoezi na kila siku alikuwa akinipatia ripoti ya mchezaji gani alikuja na nani hakuja. Katika siku 10, Ibrahim Ajibu alikuja kwenye mazoezi siku nne".
"Tulicheza mechi tatu za kirafiki na katika mechi mbili Ajibu hakucheza, hakuonekana, na mimi nikasema wakati narudi na anakuja kufanya mazoezi, siwezi kumchezesha mchezaji ambaye hafanyi mazoezi. Napenda hata kama nikifungwa na wachezaji wenye nidhamu " aliongeza kocha huyo."