Mashabiki Yanga wabakiza watoto 88 shuleni

Ijumaa , 2nd Aug , 2019

Umoja wa mashabiki wa klabu ya Yanga umekamilisha zoezi la kutoa tauloza Kike “Pedi” ili kusaidia ugawaji wa taulo hizo kwa wanafunzi wa kike waliopo shuleni.

Zoezi la kukabidhi taulo hizo kutoka Umoja wa mashabiki wa klabu hiyo kupitia makundi ya Whatsapp, umefanyika katika ofisi za EATV/Radio, Mikocheni Jijini Dar es Salaam, ambapo wamechangia jumla ya shilingi milioni 2,640,000.

Akizungumza kwa niaba yao, Katibu wa Umoja wa Makundi ya Whatsapp kwa Mashabiki, Venance Matthew Matei amesema, “Umoja wa makundi ya Whatsapp wa Yanga kutoka ndani na nje ya Tanzania liitwalo 'Yanga Whatsapp Group Admin' ambalo Mimi ndio katibu pamoja na wanachama wenzangu, tumechangia kupatikana kwa taulo hizi za kike zenye thamani ya shilingi 2,640,00”.

Yanga hivi sasa iko katika maandalizi ya mwisho kuelekea kwenye kilele cha kampeni ya 'Wiki ya Wananchi' ambapo pamoja na mambo mengine wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali kwa jamii.

Aidha kwa upande wa ugawaji wa taulo hizo za kike kwa wanafunzi walipo shuleni kwa sasa limefikia katika mikoa ya Arusha na Manyara.