AFC Leopards ilitinga fainali baada ya kuwafunga mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kwa penalti 4-2 katika mechi ya hatua ya nusu fainali wakati Gor Mahia iliichapa Nakuru All Stars mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Zedekiah Otieno, amesema wamekuja Dar es Salaam kwa kazi moja ya kusaka ubingwa na kuchukua tiketi ya kucheza na Everton FC inayoshiriki Ligi Kuu England.

"Tutafanya juhudi na kila linalowezekana ili kushinda kikombe, ni mechi ngumu lakini tunatakiwa kuongeza umakini, nataka wachezaji wangu watumie vizuri nafasi zote watakazotengeneza, ni fainali hivyo atakayefanya kosa atampa faida mpinzani wake," alisema kocha huyo.
Timu itakayoibuka mshindi katika mchezo wa leo itazawadiwa kitita cha Dola za Marekani 30,000 na ile itakayokuwa imefungwa itaambulia Dola za Marekani 10,000 wakati Yanga na Nakuru All Stars zilizotolewa katika hatua ya nusu fainali tayari zimekabidhiwa Dola za Marekani 5,000 kila moja na medali za shaba.
Waziri wa Vijana wa Kenya na mwenyeji wake Anthony Mavunde wanatarajia kuhudhuria fainali hiyo.
