Ijumaa , 31st Jul , 2020

Uongozi wa klabu ya Yanga umekamilisha usajili wa kiungo mkabaji Zawadi Mauya kutoka klabu ya Kagera Sugar

Kiungo Zawadi Mauya (Kati kati) akiwa na viongozi wa Yanga, Hersi Said ambaye ni makamu mwenyekiti kamati ya mashindano(Kushoto) na Kaimu Katibu wa klabu hiyo Patrick Simon (Kulia) wakati wa ukamilisho wa usajili.

Mauya amemwaga wino wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria wa ligi kuu ya kandanda Tanzania bara.

Nyota huyo amesaini mbele ya Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Simon Patrick na Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM, Mhandisi Hersi Saidi ambaye pia ni kaimu mwenyekiti wa kamati ya mashindano wa Yanga.

Kutua kwa Mauya ambaye anacheza idara ya kiungo, ni ishara mbaya kwa nahodha wa timu hiyo Papii Kabamba Tshishimbi ambaye amezua gumzo kufuatia kupishana na viongozi wa wanajangwani hao juu ya makubaliano ya mkataba mpya.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Mwanasheria Patrick Simon alisema hawatomlazimisha Tshishimbi kusaini mkataba mpya iwapo anaona ofa waliyompatia haimfai, na wapo tayari kusaka wachezaji wengine ambao wana uwezo kama wake.

Vile vile mapema leo zilisambaa katika mitandao ya kijamii picha za mlindalango wa Kagera Sugar Ramadhan Charamanda akiwa ameshika kinachoonekana kuwa mkataba wa klabu ya Yanga.

Bado hakuna taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Yanga kuthibitisha kama Charamanda amesajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria.

Kwani hakuonekani kuwa na changamoto katika eneo la golikipa, Metacha Mnata, Farouk Shikhalo na Ramadhani Kabwili wanaonekana kutosha.