Jumapili , 29th Jul , 2018

Mabingwa watetezi wa michuano ya Sprite Bball Kings, timu ya Mchenga Bball Stars wameanza vyema mechi zao za nusu fainali kwa kuwafunga Portland kwenye mchezo uliomalizika usiku huu kwenye uwanja wa taifa wa ndani.

Timu ya Mchenga Bball Stars

Mchenga Bball Stars walianza kwa kuongoza mchezo kuanzia Quarter ya kwanza hadi ya 4 hivyo kumaliza mchezo wakiongoza kwa pointi 70 dhidi ya 54 za Portland.

Katika nusu fainali hiyo ya kwanza kati ya 3 za 'Best of three' mchezaji wa Mchenga Bball Stars Baraka Sadick amekuwa kinara wa mchezo baada ya kufunga pointi 26, rebound 6 na Assist 3. 

Kwa upande wa Portland Yusuf Isack amefunga pointi 11 na kuchukua rebound 7 huku akitoa Assist 1. Mchenga sasa wanahitaji kushinda mechi yao ya pili ili kutinga fainali huku Portland wakihitaji kuwazuia kwa kushinda mechi yao ya pili na kusubiri mechi ya tatu ili kuamua mshindi.

Mechi za nusu fainali ya pili ya Sprite Bball Kings inayodhaminiwa na kinywaji cha Sprite, zitapigwa Jumamosi ijayo Agosti 4, 2018, ambapo Flying Dribblers watakipiga na Team Kiza ambao leo wamewafunga pointi 84 kwa 75.