Jumatano , 2nd Feb , 2022

Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania KMC FC dhidi ya Biashara United ya Mkoani Mara uliopangwa kuchezwa Ijumaa Februali 4, 2022 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, umesogezwa mbele na sasa utachezwa siku ya Jumamosi Februali 5, 2022 katika Uwanja wa Azam Complex saa 10:00 jioni.

(Kikosi cha Biashara United Mara (Juu) na kikosi cha KMC)

Kwa mujibu wa barua iliyotumwa na Bodi ya Ligi (TPLB) imeeleza kuwa awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa siku ya Ijumaa katika uwanja wa Uhuru na kwamba mabadiliko hayo yametokana na kuwepo kwa ukarabati wa miundombinu ya uwanja huo ambao unaendelea kwa sasa.

Aidha barua hiyo pia imeeleza kuwa siku hiyo ya Ijumaa ya Februali 4, 2022 katika uwanja wa Azam Complex pia kutakuwa na shughuli nyingine ikiendelea na hivyo kuamua kuusogeza mbele mchezo huo siku ya Jumamosi kwa muda wa saa 10:00 jioni.

Klabu ya KMC imepokea kwa mikono miwili mabadiliko hayo na kwamba mashabiki ambao walikua wamejiandaa kwa ajili ya kushuhudia burudani safi kutoka kwa vijana wa Kino Boys kwenye uwanja wa Uhuru wajiandae kwa ajili ya kwenda kuwasapoti kwenye uwanja wa Azam Complex kama ambavyo barua ya TPLB Ilivyo elekeza.