Alhamisi , 24th Mar , 2016

Timu nne za wasichana za mchezo wa criketi toka mikoa minne ya Tanzania bara zinataraji kuchuana mwishoni mwa wiki hii katika mashindano ya mkoa yatakayofanyika jijini Tanga kuanzia Machi 26 mwaka huu.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya criketi ya wasichana ya Tanzania katika picha.

Mjumbe wa kamati ya ufundi na mashindano ya chama cha mchezo wa criketi nchini Tanzania TCA Kharil Rhemtulah amesema mashindano hayo ya mkoa yatakayofanyika kwa siku nne yatashirikisha timu za kombaini za wasichana kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na wenyeji Tanga.

Rhemtulah ambaye kitaaluma ni kocha wa mchezo huo amesema lengo kubwa la kuwakutanisha wasichana hao ni pamoja na kutaka kuibua vipaji vipya vya wachezaji bora watakaowaongeza katika kikosi cha timu ya taifa ya wasichana ya mchezo huo nchini ambayo baadae itakwenda mjini Harare Zimbabwe kushiriki michuano ya kufuzu kucheza kombe la dunia.

Aidha Rhemtulah ameongezaq kusema kuwa wanaimani kupitia mashindano hayo watapata wachezaji bora na wenye uwezo wakukabiliana na ushindani wa aina yoyote katika michuano hiyo ya Zimbabwe kwakuwa wanaimani kubwa kila timu itakayoshiriki katika michuano hiyo ya mkoa imejiandaa vema kutoa ushindani kitu ambacho kitawarahisishia wao kama kamati ya ufundi kung'amua wachezaji bora na wenye uwezo wa hali ya juu hasa kutokana na ushindani utakaojitokeza katika mashindano hayo ya mkoa msimu huu.

Wakati huo huo timu ya kombaini ya mchezo wa criket ya mkoa wa Dar es Salaam inataraji kuondoka alfajili ya kesho kuelekea jijini Tanga kwaajili yakushiriki mashindano ya ligi yamkoa ya mchezo wa criketi yatakayoanza machi 26 mwaka huu.

Wakizungumza wakati wa mazoezi ya mwisho ya timu hiyo hii leo kocha wa Dar Kombaini Khasim Nassoro na nahodha wa timu hiyo Winfrida Kelvin wamesema timu hiyo iko tayari kwa mashindano hayo huku wakijinasibu kutwaa ubingwa wa michuano hiyo hasa kutokana na maandalizi mazuri na ya muda mrefu waliyofanya na pia wakichagizwa na ubora na vipaji vya wachezaji wa timu hiyo ambao wanauzoefu wa kutosha wakushiriki michuano mbalimbali mikubwa.

Winfrida amesema yeye kama nahodha wa timu hiyo anamatumaini makubwa ya kutimiza malengo yote waliyojiwekea msimu huu ikiwemo kutwaa ubingwa lakini kubwa ni kutoa idadi kubwa ya wachezaji watakaoteuliwa katika kikosi cha timu ya taifa itakayokwenda nchini Zimbabwe kuliwakilisha taifa katika michuano yakusaka tiketi ya kucheza mashindano ya kombe la dunia.