Jumapili , 1st Jul , 2018

Wanafainali wa mashindano ya Sprite Bball Kings mwaka uliopita timu ya TMT ambayo ilifungwa na Mabingwa Mchenga Bball Stars, jana imetoka kwenye hatua ya mchujo hivyo kushindwa kuingia kwenye 16 bora.

Wachezaji wa timu ya TMT waliovaa jezi nyeusi wakati wa mchezo wao na Street Ballers wenye jezi za blue.

Akiongea baada ya kutangazwa kwa timu 15 zilizofuzu kuungana na Mchenga Bball Stars kwenye 16 bora huku wao wakiwa hawapo, mchezaji wa TMT Reuben Ndege maarufu Nchakalih amesema mipango yao ni kuendelea kujifua vyema na kuendelea na mashindano mengine hku wakiisubiri Sprite Bball Kings msimu ujao.

''Ni kweli mimi na timu yangu tumecheza vyema lakini tofauti yetu ya pointi na wapinzani wetu Street Ballers haikuwa kubwa sana hivyo tumekosa nafasi lakini huu sio mwisho tutajipanga tena na tutafanya vizuri msimu ujao'', alisema Nchakalih.

Katika mechi yake ya mchujo jana TMT ilishinda kwa pointi 27 dhidi ya 23 Street Ballers hivyo kuwa na tofauti ya pointi 4 ambazo ni chache ukilinganisha na pointi zilziopata timu nyingine hivyo TMT ikaaga michuano katika hatua ya awali kabisa.

Nchakalih pia hakusita kusifu maandalizi mazuri yaliyofanywa na waandaaji ambao ni East Africa Television kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite. Pia aliwapongeza wachezaji wa Street Ballers kwa kuonesha kiwango kizuri.