Jumatatu , 22nd Jun , 2020

Kikosi cha wekundu wa msimbazi Simba kimewasili salama jijini Mbeya tayari kwa matayarisho kwa michezo miwili ya Ligi Kuu ya Kandanda Tanzania bara VPL dhidi ya watakaokua wenyeji wao Mbeya City na Tanzania Prisons.

Jonas Mkude (kushoto), Rais Magufuli akikabidhi kombe la ligi masimu 2017/18 (kulia)

Wekundu hao wa msimbazi ambao wanahitaji alama 8 ili kuutwaa ubingwa wa VPL bila ya kuzingatia matokeo ya wapinzani wake wa karibu, wamewasili na kikosi chenye wachezaji 20 akiwemo kiungo wake mahiri Jonas Mkude aliyekua majeruhi.

Akizungumza na kipindi cha michezo cha Kipenga ya Eas Africa Radio kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa saa mbili hadi tatu usiku, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema Mkude anaendelea vizuri baada ya kuumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya KMC, na ni uamuziwa kocha kumtumia katika mechi ya Jumatano.

Vilevile Ibrahim Ajibu ambaye amekua akikosa nafasi ya kucheza katika mechi mbili zilizopita, amejumuishwa kikosini na huenda akacheza katika mechi hizo za nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Wekundu wa msimbazi Simba wamejikusanyia alama 75 na iwapo watashinda mechi dhidi ya Prisons na Mbeya City watafikisha alama 81, na iwapo Azam na Yanga watapata sare mechi zao zijazo huenda Simba akatangazwa bingwa katika ardhi ya Mbeya.

Azam na Yanga ziligawana alama jana baada ya suluhu na kuziacha timu hizo zikiwa na alama 58 huku Yanga wakiwa na alama 56, na iwapo watashinda mechi zao zote zilizosalia watafikisha alama 82 kwa Azam na Yanga itaishia na alama 80.