Ijumaa , 19th Jun , 2020

Uongozi wa klabu ya soka ya Yanga umesema hauna nia ya kumtukuza mchezaji kutokana na ubora wake kwa kuwa taasisi ya klabu hiyo ni kubwa kuliko mtu yoyote.

Bernard Morrison akimtoka mchezaji wa wa Transit Camp

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Wakili Patrick Simon akizungumzia adhabu walizotoa dhidi ya nyota wao wa kigeni Lamine Moro aliyeonesha utovu wa nidhamu katika mechi dhidi ya JKT Tanzania, na Benard Morrison aliyeshindwa kusafiri na klabu katika mikoa ya Shinyanga na Dodoma.

Akizungumza na Kipenga ya East Africa Radio kinachoruka kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa saa mbili usiku, Wakili Patrick amesema Yanga haiungi mkono mchezo hatarishi kwa kuwa mpira wa miguu sio vita, pia haijafurahia kumkosa Lamine Moro katika mechi tatu zijazo kwa kuwa kunaweza kuigharimu timu.

Simon Patrick amesema klabu imemuadhibu nyota huyo kutokana na kanuni na sheria zilizopo, ingawa amesisiza kuwa hafahamu kama viongozi waliopita walikua wanatoa adhabu kwa wachezaji wengine waliokiuka kanuni zilizowekwa.

Kuhusiana na Bernard Morrison, Wakili Patrick amesema alizungumza naye na alimsamehe kwa kuwa alikua na hoja za msingi lakini amesisitiza kwamba maamuzi ya kumsamehe si kutokana na hadhi yake.

Amesema "Morrison ni mchezaji wa kawaida kama wachezaji wengine, Yanga ni kubwa kuliko yeye na hakuna aliyemfahamu mchezaji huyo wa Ghana kabla ya kusajiliwa na klabu yetu"