Jumapili , 18th Nov , 2018

Watanzania pande zote duniani, leo wameungana katika kuiombea dua timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika mchezo wake wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika dhidi ya Lesotho hii leo.

Kushoto ni Msanii wa Hiphop Mwana FA, katikati ni mwanamitindo Flaviana Matata na kulia ni Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Stars inazisaka alama tatu muhimu ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa asilimia 100 michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Cameroon kwa jumla ya alama nane, huku isubiri kumaliza mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda ambao hautokuwa na madhara yoyote endapo itashinda mchezo wa leo.

Mastaa mbalimbali kutoka pande zote wameonesha uzalendo mkubwa na kuguswa na mchezo huo, wakiiombea Stars kuibuka na ushindi utakaoweka historia ya kushiriki mara ya pili kwa Tanzania kwenye michuano hiyo.

Mbwana Samatta ambaye ni nahodha wa Taifa Stars atakosekana katika mchezo huo kutokana na kuoneshwa kadi mbili za njano kwenye michezo miwili mfululizo. Katika kuiombea timu yake ameandika,

"Mungu baba tunakuomba utupe sisi ata goli moja wao uwanyime, ila ata ukitupa mawili nayo sio mbaya baba, ata uwe mduki wa Msuva ata kichwa cha Bocco sisi baba fresh kabisa au baba fanya ata miujiza Ulimwengu afunge na kushoto baba ata Aishi akiubutua uingie moja kwa moja baba yetu ameen ", ameandika katika ukurasa wake wa Twitter.

Msanii nguli wa muziki wa HipHop nchini, Mwana Fa naye ameitakia kila la heri Taifa Stars katika mchezo huo kwa kuandika, "Ona pamoja na kelele zote hizi za mpira sijawahi kuiona nchi yangu ikicheza fainali za kombe la Africa TOKA KUZALIWA. Tupo karibu sana na Cameroon 2019 safari hii, karibu mno..Kwa uwezo wa Mungu, tuvuke kamlango haka..bahati njema brothers, tupelekeni Cameroon."

Mwanamitindo wa Tanzania anayeishi nchini Marekani, Flaviana Matata ameonesha uzalendo kwa taifa lake kwa kuandika, "Good luck to Taifa Stars, AFCON2019", katika ukurasa wake wa Twitter.

Taifa Stars imeshiriki mara moja pekee katika michuano ya mataifa ya Afrika, ambayo ni mwaka 1980 nchini Nigeria. Nafasi ya mwaka huu ni nafasi pekee ambayo itaweka historia kwa mara ya pili kushiriki michuano hiyo baada ya takribani miaka 38.