Jumatano , 6th Nov , 2019

Kocha mpya wa klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwasa amezungumza kwa mara ya kwanza na wachezaji wa klabu hiyo baada ya kuteuliwa jana, Novemba 5.

Kocha Charles Boniface Mkwasa na baadhi ya wachezaji wa Yanga.

Mkwasa ambaye aliwahi kuifundisha klabu hiyo kwa vipindi vitatu tofauti, amerejea baada ya uongozi kumfuta kazi kocha Mkongo, Mwinyi Zahera pamoja na benchi lake la ufundi.

Akizungumza mbele ya wachezaji hao, Mkwasa amesema, "lengo la kwanza la kila mchezaji anaekuja hapa ni kuhakikisha Yanga inabeba ubingwa. Ni lazima tuanze kushinda mechi zetu."

"Hamtachukiwa na mashabiki kama mtacheza vizuri na kushinda. Maisha yenu yatakua mazuri sana. Watu watakuja viwanjani na mtalipwa kwa wakati, nyie ni wachezaji wazuri sana na mimi niko hapa kuwasaidia kulifanikisha hilo.", ameongeza Mkwasa .

Charles Boniface Mkwasa sio mgeni katika klabu ya Yanga, alianza kuichezea klabu hiyo mwaka 1979 akitokea Mseto ya Morogoro na  alikuwa nahodha wa Yanga kuanzia mwaka 1986 hadi 1989 alipostaafu.

Mwaka 1991 alirudi kuwa kocha msaidizi chini ya kocha Syllersaid Mziray hadi mwaka 1993 na kuondoka. Alirejea tena mwaka 2001 ambapo alikuwa kocha mkuu wa Yanga hadi 2002 kabla ya kuondoka kwa mara ya pili kama kocha. Baada ya hapo alirudi mwaka 2013 kama kocha msaidizi wa Hans van der Pluijm hadi mwaka 2015.