Jumamosi , 2nd Aug , 2014

Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema anakiamini kikosi chake ambacho kesho (Agosti 3 mwaka huu) kinacheza mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji (Mambas).

Kikosi cha taifa stars ambacho kesho kitaivaa Mambaz ya Msumbiji.

Mechi hiyo ndiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya Tanzania na Msumbiji itakayoingia hatua ya makundi ya michuano ya Afrika kwa ajili ya kutafuta tiketi za Fainali itakayofanyika mwakani nchini Morocco.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Timu itakayosonga mbele itaingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia.

Akizungumza kutoka jijini Maputo, Nooij amesema anaamini kikosi chake kitacheza vizuri zaidi kuliko kilivyofanya jijini Dar es Salaam kwa vile hakitakuwa katika shinikizo la mashabiki ambao mara nyingi hufanya wachezaji wasijiamini

Taifa Stars itafanya mazoezi leo (Agosti 2 mwaka huu) saa 9 Alasiri Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi ya kesho.

Kikosi hicho cha timu ya Taifa leo kimeandaliwa chakula cha jioni na Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Shamim Nyanduga

Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu nao wameungana na timu leo asubuhi hapa Maputo wakitokea Lubumbashi katika klabu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Uganda wakiongozwa na Dennis Batte itaanza saa 9 Alasiri kwa saa za Msumbiji ambapo nyumbani Tanzania itakuwa saa 10 jioni.

Wachezaji waliopo katika kikosi cha Taifa Stars hapa Maputo ni Aggrey Morris, Aishi Manula, Amri Kiemba, Deogratias Munishi, Erasto Nyoni, Haruna Chanongo, Himid Mao, John Bocco, Kelvin Yondani, Khamis Mcha, Mbwana Samata, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub, Oscar Joshua, Ramadhan Singano, Said Moradi, Shabani Nditi, Shomari Kapombe, Simon Msuva na Thomas Ulimwengu.