Nyundo zitakazoshusha daraja klabu msimu ujao

Jumanne , 24th Mar , 2020

Wakati huu shughuli za soka zikiwa zimesitishwa nchini Tanzania, Bodi ya Ligi (TPBL) imeendelea kutoa semina kwa klabu mbalimbali nchini juu ya majadiliano kuhusu suala la leseni za klabu.

Rais wa TFF, Wallace Karia na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo

Katika ziara iliyofanyika mkoani Mbeya hivi karibuni, timu ya Bodi ya Ligi ikiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo ilikutana na klabu mbalimbali mkoani humo kwa ajili ya kujadiliana kwa pamoja kuhusu suala hilo.

Baada ya kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu amesema kuanzia msimu ujao, timu zitakazoshindwa kufuata matakwa ya leseni za klabu, hazitapewa leseni ya kushiriki ligi yoyote nchini.

"Tumekaa na klabu mbalimbali hapa Mbeya na kujadiliana kuhusu matakwa wanayohitajika kuyafuata ili kupata leseni kwa mujibu wa FIFA", amesema Kasongo.

"Kuanzia msimu ujao klabu zinatakiwa kuwa na Mtendaji Mkuu, Bwana fedha mwenye taaluma, Afisa Habari mwenye sifa, Vilabu visidaiwe na wachezaji, Vilabu viwe na ofisi kamili, Kiwanja cha mazoezi na kingine na mechi, Afisa usalama atakayeshirikiana na Bodi ya Ligi na Afisa Masoko", ameongeza.

Pia Kasongo akasisitiza kuwa vigezo hivyo vinapaswa kufuatwa na klabu zote zilizo chini ya Bodi ya Ligi na kwamba klabu zitakazoshindwa kutimiza, hazitapewa leseni na kama hazitapewa leseni maana yake hazitakuwa na sifa ya kucheza ligi.