Jumanne , 15th Jul , 2014

Rais Jakaya Kikwete amewataka wanamichezo wa Tanzania wanaotaraji kutuwakilisha katika michuano ya jumuiya ya madola, kuhakikisha wanapambana vyakutosha na kwa uwezo wao wote ili waweze kurejea na medali katika michuano hiyo

Rais Jakaya Kikwete akiwa na baadhi ya viongozi pamoja wachezaji wa Tanzania watakaoshiriki michuano ya madola.

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amewataka wanamichezo wa Tanzania wanaotaraji kutuwakilisha katika michuano ya jumuiya ya madola itakayofanyika jijini Grascow Scotland kuanzia July 23 mwaka huu wahakikishe wanapambana vyakutosha na kwa uwezo wao wote ili waweze kurejea na medali katika michuano hiyo

Rais Kikwete amesema hayo wakati wa hafla ya kuwaaga walimu 8 na wanamichezo 39 wa michezo ya riadha, judo, ngumi kuogelea, mpira wa meza na kunyanyua vitu vizito ambao walikua nje ya nchi katika kambi maalumu ya mafunzo ya maandalizi ya michuano ya jumuiya ya madola

Aidha Rais Kikwete amesema kwa maandalizi ya safari hii waliyopata wanamichezo hao kutoka katika kambi nje ya nchi katika nchi za Ethiopia, Uturuki, China na New zealand hategemei kisingizio cha aina yoyote kutoka kwa wanamichezo hao na kilichobaki kwa watanzania ni kuwaombea dua ili waweze kupeperusha vema bendera ya Taifa

Naye naibu waziri wizara ya habari utamaduni vijana na michezo Mh. Juma Nkamia wakati akimkaribisha Rais Kikwete amewaambia vijana wote ambao watatuwakirisha katika michuano hiyo wako tayari na wanauhakika watarejea na medali nyingi kutokana na maandalizi waliyopata

Aidha Mh. Nkamia ametoa pongezi kwa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa kwakufanikisha maandalizi ya wanamichezo hao kwa ushirikiano na wizara yake,

Kwa upande mwingine Rais wa kamati ya Olimpiki Tanzania TOC Ghuram Rashid kwa niaba ya wanamichezo na vyama vya michezo ameiomba serikali kuhakikisha wanatoa fursa kama hiyo mara kwa mara kwa wachezaji kwenda kuweka kambi za maandalizi nje ya nchi hasa wanapokabiliwa na mashindano makubwa kama ya jumuiya ya madola
Ghuram amesema kwa maandalizi waliyopata wanamichezo hao ambao kesho wanaondoka kwenda katika michuano hiyo ana uhakika watafanya maajabu huko Scotland mwaka huu

Na mara baada ya kukabidhiwa bendera ya taifa nahodha wa timu ya jumuiya ya madola ya Tanzania mwanamasumbwi Suleiman Kidunda amemwahidi mh. rais Jakaya Kikwete na watanzania wote kwa ujumla kuwa watarejea na medali katika michuano hiyo na hivyo wanachoomba ni dua za watanzania ili waweze kufanya vema na kutimiza adhma hiyo.