Jumatatu , 21st Jun , 2021

Baada ya timu ya taifa ya Italia kutopewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa michuano ya mataifa barani Ulaya Euro 2020, kabla ya michuano kuanza Juni 11 sasa timu hiyo inatazamwa kwa jicho la tofauti baada ya kushinda michezo yote mitatu ya makundi.

wachezaji wa Italia wakishangilia kwenye mchezo dhidi ya Wales

Azzurri chini ya kocha Roberto Mancini imeshinda michezo yote mitatau ya awali kwenye mashindano hayo pasipo kuruhusu bao wakishinda dhidi ya Wales, Uturuki na Uswisi kwenye michezo ya kundi A'. na sasa timu hiyo imecheza michezo 30 mfululizo pasipo kupoteza na wameshinda michezo 11 ya mwisho mfululizo pasipo kuruhusu bao huku wakiwa wamefunga jumla ya mabao 32 kwenye michezo hiyo.

Mara ya mwisho timu hiyo kushinda michezo yote ya hatua ya makundi ilifika mpaka hatua ya fainali na ilipoteza dhidi ya Ufaransa, ilikuwa kwenye finali za Euro mwaka 2000 ambapo walipoteza kwa mabao 2-1.

Italia imeshinda michezo yake kwa ushawishi mkubwa licha ya kuonekana wanacheza dhidi ya timu dhaifu, lakini walau wamepata matokeo dhidi ya timu wanazozimudu, tofauti hata na timu ambazo zinapigiwa upatu kutwaa ubingwa kama England ambao walilazimishwa sare na Scotland, Ufaransa pia walibanwa mbavu na Hungary, Ureno mabingwa watetezi walipigwa na Ujerumani lakini Ujermunai nayo ilipoteza mchezo wa kwanza.

Mara ya mwisho timu hiyo kutwaa taji kwenye mashindano makubwa ilikuwa mwaka 2006 ambapo walikuwa mabingwa wa Dunia, kwa sasa kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wenye uzoefu na vijana kama Nicolo Barella, Manuel Locatelli na Federico Chiesa pamoja na wenye uzoefu Francesco Acerbi, Giorgio Chiellini na Leonardo Bonucci.

Na hatua ya inayofata ya 16 bora watacheza na timu itakayomaliza nafasi ya pili kutoka kundi C kati ya Austria au Ukraine.