
Mbwana Samatta
Katika mchezo wa ligi kuu nchini Ubelgiji wikiendi iliyopita, Samatta aliifungia bao la pili timu yake, KRC Genk iliposhinda kwa mabao 2-0 dhidi ya KV Oostende katika uwanja wake wa nyumbani wa Luminus Arena mjini Genk.
Samatta alifunga bao hilo dakika ya 74, ambapo ushindo huo unaifanya KRC Genk kufikisha pointi 42 baada ya kucheza mechi 19, ikiizidi Club Brugge inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 7.
Samatta anaongoza katika listi ya wafungaji bora wa ligi hiyo maarufu kama 'Jupiter Pro Legue' akiwa na mabao 12, akikimbizana na mastaa kadhaa barani Ulaya kama Lionel Messi mwenye mabao 14 kwenye La Liga, Mohamed Salah mwenye mabao 10 katika EPL na Cristiano Ronaldo ambaye amefunga mabao 11 katika Serie A.
Nahodha huyo wa Taifa Stars pia amecheza mechi 134 katika mashindano yote tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa jumla ya mabao 53. Katika Ligi ya Ubelgiji pekee amefikisha mechi 104 na kufunga mabao 38, Kombe la Ubelgiji mechi nane na mabao mawili na Europa League akiwa amecheza mechi 22 na kufunga mabao 14.
Katikati ya miezi ya Septemba na Oktoba kulikuwa na tetesi zinazomuhusisha nyota huyo kutaka kusajiliwa na klabu kadhaa barani Ulaya hasa za ligi kuu ya Uingereza EPL.
Dirisha la usajili barani Ulaya linatarajiwa kufunguliwa mwezi Januari, tusubiri na kuona kama ndoto za Mbwana Samatta kucheza soka hasa katika EPL itatimia.