Jumanne , 21st Mei , 2019

Klabu ya soka ya Simba imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2018/19, baada ya kuifunga Singida United magoli 2-0 na kufikisha pointi 91, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Kikosi cha Simba na Kocha Patrick Aussems

Simba imechukua ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo, huku baadhi ya wachezaji wake wakiweka rekodi mbalimbali katika misimu kadhaa waliyocheza klabuni hapo.

Mshambuliaji wa Simba Meddie Kagere amekuwa mchezaji wa kwanza kutwaa ubingwa na Simba akiwa kwenye msimu wake wa kwanza akiwa na magoli 23 ya kufunga rekodi ambayo haikuwahi kuwekwa hapo kabla.

Kwa upande wa John Bocco na Aishi Manula, wamejiwekea rekodi ya kushinda ubingwa wa ligi mara mbili mfululizo wakiwa kwenye timu yao mpya ya Simba huku wakiwa wametoka kwenye timu moja ya Azam FC.

Kwa upande wa mchezaji wa kimataifa mkongwe katika kikosi hicho Emmanuel Okwi yeye amefikisha mataji manne ya ligi kuu akiwa na Simba tangu alipojiunga nayo. Alitwaa mwaka 2011, 2012, 2018, 2019.

Simba wenyewe wameweka rekodi ya kuchukua ubingwa wao mfululizo kwenye uwanja wa Namfua wakicheza na Singida United ambapo msimu uliopita walitwaa ubingwa kwa kushinda 1-0 palepale Namfua.

Kwa upande wa Haruna Niyonzima ameweka rekodi ya kushinda taji mara 5 mfululzo baada ya kushinda mara tatu akiwa na Yanga na sasa mara mbili akiwa na Simba.

Rekodi nyingine ya Simba ni kushinda mechi zote 4 dhidi ya Singida United katika misimu miwili ambayo timu hiyo imerejea ligi kuu. Walishinda 4-0, 1-0, 3-0 na leo 2-0.