Ijumaa , 16th Nov , 2018

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) imeondoka nchini Afrika Kusini leo kuelekea Lesotho ambako itacheza mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2019 dhidi ya Lesotho ambapo nahodha Mbwana Samatta ataungana na timu licha ya kuwa majeruhi.

Mbwana Samatta

Akiongea na www.eatv.tv mapema leo kabla ya timu kuondoka nchini humo, meneja wa timu hiyo Danny Msangi, amesema kikosi kipo tayari kwa mchezo huo na wachezaji wote wa kimataifa wameungana na timu isipokuwa nahodha Mbwana Samatta.

''Wachezaji wote wako vizuri isipokuwa Shomari Kapombe na Rashid Mandawa ambao watakosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi lakini pia tunataraji nahodha Mbwana Samatta ataungana na timu nchini Lesotho akitokea Dar es salaam ambako alikwenda kutokana na matatizo ya kifamilia'', amesema Msangi.

Samatta ambaye alifunga bao la pili kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde jijini Dar es salaam hatakuwa sehemu ya mchezo huo kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

Taifa Stars ina alama 5 kwenye nafasi ya pili Kundi L ikiwa nyuma ya Uganda yenye alama 10 na ikifuatiwa na Cape Verde ambao wapo katika nafasi ya 3 wakiwa na alama 4. Mchezo utapigwa Jumapili Uwanja wa Setsoto mjini Maseru kuanzia Saa 11:00 jioni.