Alhamisi , 6th Apr , 2017

Serikali imetangaza kurejesha michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi (UMITASHUMTA) na shule za sekondari (UMISETA) kuanzia mwaka huu baada ya kuisitisha mwaka jana.

Ufunguzi wa Mashindano ya UMISETA mwaka 2015

Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni mjini Dodoma, ambapo amesema mashindano hayo yanarudi na yatafanyika kitaifa mkoani Mwanza kama ilivyokuwa imepangwa awali.

"Mh. Spika, mwaka huu mashindano kwa shule za msingi na sekondari yanarudi na yatafanyika mkoani Mwanza, nawaagiza wahusika wote wafanye matayarisho" Amesema Majaliwa.

Ikumbukwe kuwa serikali kupitia Waziri wa TAMISEMI, Mh. George Simbachawene, mwaka jana alitangaza kusitisha mashindano hayo kwa muda usiojulikana, katika kipindi ambacho wahusika (wanafunzi, wachezaji na walimu) walikuwa tayari wamekwisha wasili Mwanza kwa ajili ya mashindano hayo.

Simbachawene alisema sababu ya kusitisha mashindano hayo ilikuwa ni kukithiri kwa ugonjwa wa kipindupindu pamoja na zoezi la madawati akidai kuwa waliokuwa wanahusika katika mashindano hayo ndiyo waliokuwa wakihusika katika zoezi lile la madawati, hivyo aliwataka walimu na watendaji wa halmashauri kuweka nguvu kwenye ukamilishaji wa zoezi la madawati kwanza kabla ya michezo hiyo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Aidha waziri mkuu pia amewapongeza timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys kwa kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana, Twiga Stars kwa kuibuka mabingwa wa CECAFA na mwanariadha Alponce Simbu kwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Mumbai Marathon.