Shughuli za soka kusitishwa Kenya

Ijumaa , 13th Mar , 2020

Shirikisho la Soka nchini Kenya FKF limeazimia kusimamisha shughuli zote rasmi za soka nchini humu baada ya uthibitisho wa kesi ya kwanza ya muathirika wa virusi vya Corona nchini humo.

Mabingwa ligi kuu Kenya

FKF tayari imesimamisha kwa muda usiojulikana mashindano yote rasmi ya vijana, mashindano ya wanawake ikiwemo ligi ya wanawake, Ligi Daraja la Kwanza pamoja na Ligi Daraja la Pili.

Ligi Kuu ya Soka nchini humo KPL itaendelea na ratiba yake wikiendi hii kwa mechi kadhaa kupigwa lakini bila ya uwepo wa mashabiki, huku agizo la kusiamamisha michezo hiyo likitarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu, Machi 16. 

Pia katika kujihadhari na virusi hivyo, shirikisho limeziagiza klabu zote nchini humo kusitisha shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko ya wachezaji, wafanyakazi wa klabu au mashabiki kama programu za mazoezi, mikutano na mikusanyiko ya mashabiki.