Ijumaa , 13th Dec , 2019

Ligi kuu ya soka ya Wanawake Tanzania Bara, kesho Desemba 14, 2019 itaendelea kwa mechi ya 4 kwa kila timu, ambapo macho na masikio ya wengi yatakuwa katika Uwanja wa TFF Karume, katika mchezo wa Derby ya Kariakoo ya wanawake baina ya Simba Queens dhidi ya Yanga Princess.

Manahodha wa Yanga na Simba pamoja na makocha

Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo makocha wa timu zote mbili ambapo kwa upande wa kocha msaidizi wa Yanga Princess Nasorro Muskini, amesema kuwa licha ya kupata ushindi wa 100% tangu kuanza ligi kwa upande wao kwa mchezo wa kesho wanauchukulia kama fainali.

"Ni kweli Simba walitufunga michezo yote miwili ya msimu uliopita wa nyumbani na ugenini lakini mtambue kuwa Yanga ya msimu uliopita na ya sasa ni tofauti ndiyo maana hatuja poteza mchezo hadi sasa wala sare" amesema kocha Nasorro.

Kwa upande wake kocha wa Simba Queen's Mussa Hassan Mgosi ametamba kufanya vyema huku akiamini kuwa wembe ulio mnyoa Yanga msimu uliopita ndio watakao utumia kumuangamiza hapo kesho.

"Malengo yetu ni kuuchukua ubingwa wachezaji wako tayari kwa mchezo uliopita kama tumeweza kumfunga JKT ambaye ni bingwa mtetezi basi tunaamini hata kesho tutafanya vizuri" Amesema Mgosi.

Naye Nahodha wa Simba Queens Mwanahamisi Omary maarufu kama "Gaucho" amesema wao kama wachezaji hawaidharau Yanga Princess, bali anaamini wamejipanga kuchukua pointi hapo kesho.

"Aliyekuwa anaongoza kwa miaka miwili mfululizo  tumeweza kumfunga hivyo hata kwa Yanga tunaimani tutapata matokeo", amesema Mwanahamisi Omary.

Yanga princess watamkosa kocha wao mkuu Edna Lema ambaye yupo Uganda kwenye mashindano ya Cecafa U17  akiwa kocha msaidizi wa timu hiyo akimsaidia Bakari Shime.

Huu ni Msimu wa nne wa ligi kuu ya wanawake, ambapo msimu wa kwanza ubingwa ulichukuliwa na Mlandizi Queens na katika misimu miwili mfululizo iliyofuata walichukua JKT Queens.