Simba yahusishwa na washambuliaji 2 Kimataifa

Jumatano , 20th Mei , 2020

Katika kipindi cha mwezi mmoja wa Mei, 2020 klabu ya Simba imehusishwa na kuwasajili washambuliaji wawili wa kimataifa ili kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa ligi pamoja na michuano ya Kimataifa.

Justin Shonga (kushoto) na Michael Sarpong (kulia)

Mwanzoni mwa mwezi Mei 2020, kulikuwepo na tetesi za Simba kuhusishwa na kumsajili mashambuliaji wa klabu ya Orlando Pirates, Mzambia Justin Shonga. Mchezaji huyo ana umri wa miaka 23 na ameichezea timu ya taifa ya Zambia takribani mechi 24 na kufunga mabao 13 tangu mwaka 2017.

Pia hivi karibuni klabu ya Simba imehusishwa na tetesi za kumsajili mshambuliaji wa klabu ya Rayon Sports raia wa Ghana, Michael Sarpong (24) ambaye ndiye alikuwa mfungaji bora wa msimu wa 2018/19 akiwa amefunga mabao 16. Pia mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na kusajiliwa na mahasimu wao Yanga.

Imeelezwa kuwa Simba imethamiria kuwa na safu bora ya ushambuliaji hasa katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika msimu ujao ili izidi katika hatua ya makundi ambayo iliishia msimu huu.

Baadhi ya wachezaji ambao wanatajwa huenda wakaachwa na Simba ili kupisha usajili huo ni pamoja na Haruna Shamte, Kennedy Juma, Tairone Santos, Shiza Kichuya, Yusuf Mlipili ambao wamekuwa hawana nafasi za kudumua katika kikosi cha kwanza.