Jumanne , 25th Dec , 2018

Klabu ya soka ya Simba imeshiriki kikamilifu katika mazishi ya mwanachama wake Kessy Rajab, ambaye alifariki Desemba 23, 2018 siku ambayo Simba ilikuwa inacheza na Nkana FC na kushinda kwa mabao 3-1 na kufuzu hatua ya 16 bora.

Viongozi wa Simba wakiwa msibani Morogoro.

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema viongozi wa Simba akiwemo yeye mwenyewe na Rais wa klabu Sweddy Mkwabi, wameshiriki mazishi hayo ambayo yamefanyika leo huko mkoani Morogoro.

''Simba iliwakilishwa vema katika msiba wa Mwanachama wetu maarufu Kessy Rajabu, mimi pamoja na Mwenyekiti Sweddy Mkwabi na Mjumbe mstaafu wa kamati ya utendaji Suru Ally'', amesema Manara.

Mbali na Simba pia shirikisho la soka nchini (TFF), limeshiriki katika msiba huo ambapo marehemu Kessy alikuwa ni mtunza vifaa msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Marehemu Kessy Rajab alifariki Jumapili kwa shinikizo la damu, ambapo imeelezwa mapema alikuwa kwenye mchezo wa Simba uwanja wa taifa kabla ya kukimbizwa hospitali ya Temeke baada ya kuumwa ghafla.