Alhamisi , 8th Jan , 2015

Simba SC imefanikiwa kuingia hatua ya Nusu fainali baada ya kuifunga timu ya Jang'ombe goli 4-0 katika mchezo wa Robo fainali uliochezwa hapo jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mshambuliaji Ibrahim Hajibu aliyekuwa akiichezea Simba B akitokea Benchi aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Awadh Juma, alifunga mabao matatu katika Dakika ya 46, 63 na 75 Kabla ya Shaaban Kisiga aliyotokea Benchi pia kufunga bao la nne katika Dakika ya 80.

Hajibu alianza kwa kufunga bao la kwanza akimalizia Krosi ya Dan Sserunkuma wakati bao la Pili alimalizia kwa kichwa Krosi ya Simon Serunkuma aliyetokea Benchi pia.

Bao la tatu la Hajibu alifunga kwa penati baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na Abdallah Hajji huku Shaban Kisiga akifunga bao lake kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya yeye mwenyewe kuangushwa umbali wa mita 26.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Beki wa Kulia wa Simba SC, Hassan Kessy alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

Simba sasa itasubiri mshindi wa mchezo kati ya Mabingwa watetezi wa Kombe hilo, KCCA ya Uganda au Polisi ya Zanzibar, katika mchezo wa Nusu fainali utakaochezwa Jumamosi.