Solskjaer amuonya mchezaji juu ya mitandao

Jumatatu , 6th Jan , 2020

Imejulikana kuwa kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer alimemueleza mshambuliaji wake Jesse Lingard aachane na matumizi ya mtandao ya kijamii ili arudishe kiwango chake kilichozorota hivi karibuni.

Kocha wa Man United na mchezaji Jesse Lingard

Jesse Lingard amekuwa na kiwango kibovu hivi sasa ndani ya klabu hiyo, akiwa hajafunga bao lolote au kutoa 'assist' katika ligi kuu ndani ya mwaka 2019, huku pia akiachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza.

Akizungumza kuelekea mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Carabao kesho Januari 7, Solskjaer amesema, "tunamuhitaji Lingard kwenye ufungaji na kutoa 'assist'. Sidhani kama Jesse anaonekana sana kwenye mitandao kwa sasa kama mlivyokuwa mkimuona hapo nyuma, anajituma kwa nguvu ili aweze kurejea yule Jesse niliyemjua".

Alipoulizwa kuhusu matumizi ya mitandao kwa wachezaji, Solskjaer amesema, "ni moja ya majukumu ya kuwa mchezaji wa Man United, ninaongea sana na wachezaji juu ya namna ya kuishi katika mitandao. Mimi sina mambo haya ya mitandao lakini kumbuka hiki ni kizazi tofauti".

Man United itawakaribisha mahasimu wao wa mji mmoja, Manchester City katika dimba la Old Trafford Jumanne hii kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la Carabao, ikiwa na majeraha kadhaa mpaka sasa akiwemo Jesse Lingard, Anthony Martial na Luke Shaw ambao walikosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Wolves, ambapo amesema mpaka kufikia mapema Jumanne atajua kama ataweza kuwatumia baadhi yao.