
Mshambuliaji wa Chelsea, Romelu Lukaku akishangilia baada ya kufunga bao lake la kwanza akiwa mchezaji wa Chelsea, kufuatia kuifunfa Arsenal dakika 15 kwenye ushindi wa 2-0 usiku wa jana.
6. Ni idadi ya mashuti yaliyolenga lango ambayo klabu ya Chelsea ilipiga kwenye mchezo wa ligi kuu England dhidi ya Arsenal mchezo ambao ulimalizika kwa Arsenal kufungwa kwa mabao 2-0 na kuifanya The Gunners kufungwa michezo miwili mfululizo ya Ligi huku ikiwa haijafunga bao hata moja kwenye michezo hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza kutokea kwa klabu hiyo, huu ikiwa ni msimu wao wa 118 wa ushiriki wa Ligi England.
Rekodi hii mbaya the Gunners wameiweka baada ya kufungwa na Chelsea kwenye mchezo wa Derby ya London kwa mabao 2-0. Na mabo ya Chlesea yalifungwa na Romelu Lukaku na Reece James.
Arsenal ilipoteza pia mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi dhidi ya Brentford kwa kufungwa mabao 2-0, Kipigo dhidi ya Chelsea kinakuwa ni cha 20 kwa kocha Mikel Artetea kwenye michezo 60 ya Ligi Kuu England EPL, nani kwa mara ya kwanza washika Bunduki hao wapo kwenye mstari wa kushuka daraja baada ya kuchezwa michezo miwili ya Ligi Tangu mwaka 1992.
5. Ni idadi ya pasi za mabao (Asissts) alizotoa kiungo wa Manchester United Paul Pogba kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu England na ndio kinara kwenye orodha ya wachezaji waliopiga pasi nyingi za mabao. Idadi hiyo ameifikia baada ya kiungo huyo wa kimataifa wa ufaransa kumpa pasi ya bao Meson Greenwood na kufunga bao la kusawazisha kwenye mchezo dhidi ya watakatifu kutoka pwani ya kusini ya England klabu ya Southampton mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Na Idadi hiyo ya pasi za za mabao (Asisst) inamfanya Pogba kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu England kutoa idadi hiyo ya pasi za mabao kwenye michezo miwili ya kwanza ya ufunguzi wa Ligi. Pogba alitoa pasi nne (4) za mabao kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi dhidi ya Leeds United mchezo ambao Manchester United ilishinda kwa mabao 5-1.
4. Ni idadi ya michezo ya kirafiki itakayocheza klabu ya Azam FC nchini Zambia ambako kikosi hicho kinaenda kuweka kambi ya maandalizi kuelekea msimu ujao wa mashindano yani Pre season, kambi hiyo itakauwa ya takribani wiki moja na nusu. Kikosi hicho cha waoka mikate wa jiji la dar es salaam kinaondoka leo Jumatatu Agosti 23 kueleka Ndola Zambia.
Michezo hiyo mine ya kirafiki ni dhidi ya Red Arrows ambayo ni timu ya jesho mchezo huu utachezwa Agosti 25, Agosti 29 wataminyana na Zanaco, mchezo wa tatu watakipiga dhidi ya Forest Rangers mchezo huu utachezwa Septemba 2 na mchezo wa mwisho watacheza Septemba 3 dhidi ya Zesco ambayo ni timu ya shirika laumeme. Na baada ya michezo hiyo kikosi cha Azam FC kitarejea nchini Septemba 5 tayari kwa mchezo wao wa kombe la shirikisho barani dhidi ya Horseed ya Mogadishu Somalia.
3 - Ni idadi ya misimu ambaye nyota wa timu ya taifa ya Uswizi, Xherdan Shaqiri almaarufu 'Kistuli' ameitumikia klabu yake ya Liverpool na kuichezea michezo 63 na kufanikiwa kuingia wavuni mara 8 na kutoa Assist 9 kwenye michezo ya michuano yote akitokea klabu ya Stoke City ya England.
Safari ya Liverpool na winga huyo mwenye msuli mnene inaelekea ukingoni na hii ni baada ya miamba ya soka nchini Ufaransa, klabu ya Lyon kukubali kutoa paundi milioni 9.5 za England sawa na bilioni 30 na zaidi ya milioni 90 za kitanzania ili kumsajili nyote huyo ambaye tayari amemuomba kocha wake Jurgen Klopp amuachie aende zake ili akapate dakika nyingi za kucheza zaidi.
2. Ni idadi ya seti alizoshinda mwanamama aAshleigh Barty anayeshika nafasi ya kwanza kwenye viwango vya ubora kwa wacheza tennis duniani upande wanawake. Mchezaji huyo raia wa Australia ameshinda taji lake la 5 ndani ya mwaka 2021 baada ya kushinda ubingwa wa michuano ya wazi ya Cincinnati kufuatia kumfunga Jil Teichmann raia wa Uswiss kwa seti 2 mfululizo 6-3, 6-1. Licha ya kupoteza mchezo wa fainali Teichmann raia wa Uswiss ambaye anashika nafasi ya 76 kwenye viwango vya ubora aliwaondoa vigogo mpaka anafika hatua ya fainali kwani aliwatoa wachezaji kama Naomi Osaka mshindi mara nne wa Grandslam, mchezaji namba 4 Karolina Pliskova na mshindi wa medali ya dhahabu kwenye Olympic Belinda Bencic.
Barty kwenye msimu huu ameshinda mataji matano ambayo ni Yarra Valley Classic, Miami Open, Sturtgart Open, Wembledon ambayo ni Grandslam na jana usiku ametwaa ubingwa waCincinnati. Barty anapigiwa upatu kutwaa ubingwa wa michuano ya wazi ya Marekani Us Open inayotarajiwa kuanza Agosti 30.
1 - Ni idadi ya msimu pekee kwenye NBA ambao timu zilicheza mizunguko 72 na si 82 kama ilivyozoeleka hapo awali huku moja ya sababu ya kupunguza idadi hiyo ya michezo kwenye regular season ya msimu uliopita mwaka 2020-2021 ilikuwa ni janga la covid-19.
Taarifa kutoka NBA zimeweka wazi kuwa kila timu itakayoshiriki kucheza NBA kwa msimu ujao wa mwaka 2021-2022 unaotarajiwa kuanza Oktoba 19 na kumalizika April 10, 2022 watarudi kwenye orodha ya michezo 82 kama ilivyozoeleka hapo awali.
Pamoja na marekebisho hayo, NBA wametangaza kutakuwa na michezo mahususi 5 ya kuendelea kuadhimisha miaka 75 tokea kuanzishwa kwa ligi hiyo mwaka 1946. Toronto Raptors watacheza dhidi ya New York Knicks kama kumbizi ya mchezo wa kufungua dimba wa NBA mwaka huo, Golden State Warriors watacheza na Boston Celtics kama timu zilizowahi kucheza kwenye misimu yote tokea kuanzishwa kwa NBA, Golden State watakipiga tena na New york knicks, New York Knicks watakipiga na Boston Celtics wakati LA Lakers watacheza na Atlanta Hawks ikiwa na rekodi pekee ya Lakers kumfunga Atlanta mara 33 mfululizo ikiwa ni mara nying zaidi kwenye historia.