Ijumaa , 13th Aug , 2021

'Sports Countdown' ya EA Radio ya Leo Agosti 14, 2021 inakupitisha kwenye kuzihesabu zile stori 6 kali za kimichezo zilizojiri na ambazo zitajiri. 'Sports Countdown' inakujia kila siku ya Jumatatu - Ijumaa saa moja na robo asubuhi kwenye 'Supa Breakfast' ya EA Radio saa 12:00-4:00 Asubuhi.

Lionel Messi akishikilia jezi ya PSG baada ya kutambulishwa kwenye klabu yake hiyo mpya.

6 - Ni idadi ya wachezaji wapya walithibitishwa na kutambulishwa na klabu ya Yanga mpaka kufikia usiku wa hapo jana. Klabu hiyo kongwe nchini imeendelea na zoezi lake la kusajili nyota wapya ambapo usiku wa kuamkia leo wamethibitisha kumsajili na kumtangaza David Bryson anayecheza mafasi ya mlinzi wa kushoto kwa kandarasi inayoaminika ya miaka miwili akitokea klabu ya KMC.

David Bryson anakuwa mchezaji watatu wakizawa na wasaba kusajiliwa na Yanga kwenye dirisha hili kubwa la Usajili huku nyota wengine watatu wakimataifa kutoka DR Congo wakitaraji kuthibitishwa kama vile Djuma Shaaban, Ducapel Jesus Moloko na Yannick Bangala.

5 - Ni idadi ya michezo ambayo mshambuliaji Romelu Lukaku mwenye miaka 28 kwasasa alifanikiwa kuichezea timu yake ya taifa ya Ubeligiji ya vijana chini ya miaka 21 mwaka 2009 na kufanikiwa kuifungia bao moja pekee.

Mkali huyo wa kupachika mabao ambaye anasifika kwa kucheza soka kwa mabavu mithili ya nyati dume, usiku wa hapo jana amethibitishwa kusajiliwa na klabu yake ya zamani ya Chelsea ya England kwa ada ya uhamisho wa rekodi kwenye klabu hiyo ya paundi milioni 97.5 sawa na Bilioni 312 na zaidi ya milioni 170 za Kitanzania akitokea Inter Milan ya Italia na kusaini kandarasi ya miaka 5  hadi mwaka 2026 na kumfanya awe mchezaji wa pili ghali kwenye ligi kuu ya England nyuma ya Jack Grealish wa Manchester City aliyesajiliwa kwa paundi milioni 100 za England sawa na bilioni zaidi ya 320 za kitanzania akitokea Aston Villa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Ikumbukwe kuwa Lukaku aliwahi kucheza michezo 15 pekee awali alivyokuwa Chelsea mwaka 2011 akiwa na miaka 17 akitokea Anderletch ya Ubelgiji kabla ya kuuzwa Everton mwaka 2014.

4 - Ni idadi ya michezo ambayo washika mitutu wa jiji la London, klabu ya Arsenal walishinda mfululizo katika michezo yake kumi ya mwisho kwenye michuano yote kwenye msimu uliopita.

Arsenal ambayo ndiyo timu pekee kwenye ligi kuu England kutwaa ubingwa bila kufungwa hata mchezo mmoja, itakuwa ndiye kigogo pekee anayefungua pazia la msimu mpya wa ligi hiyo maarufu EPL kwa msimu wake wa 30 saa 4 usiku wa leo Agosti 13 itakapokipiga na Brentford iliyopanda daraja baada ya majaribio 9 kwenye dimba la Brentford Community.

Mara ya mwisho wawili hao kukutana ilikuwa Juni 10 mwaka huu kwenye mchezo wa kirafiki ambapo Arsenal alifungwa 3-2.

Na ligi hiyo itaendelea wikiendi hii ambapo bingwa mtetezi Manchester City atacheza na Spurs saa 12:30 jioni siku ya Jumapili ya Agosti 15.

3 - Ni idadi ya siku zilizopita tokea wekundu wa Msimbazi Simba uondoke nchini kwenda Morocco kuweka kambi inayotaraji kuwa ya siku 14 kabla ya kurejea nchini na kuhitimisha kilele cha bonanza la Simba Day.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mfaransa, Didier Gomes Da Rosa ametoa ripoti ya mapema baada ya kikosi chake kufanya mazoezi ya kwanza baada ya kuwasili nchini humo hapo jana. Gomes amesema wanafuraha sana kuwepo nchini humo kwa sababu mazingira ya kazi ni mazuri kwani wanafanya mazoezi uwanjani pamoja na kwenye gym na mwisho kusema anataraji jioni ya leo Agosti 13 ataungana na kundi la pili la wachezaji huku wapinzani wao Yanga wakitaraji kusafiri Jumapili ya Agosti 15, 2021 kuelekea nchi Morocco.

2 - Ni idadi ya medali za ushindi alizozitwaa mwanariadha Chijindu Ujah baada ya kushinda mbio za mita 400 akiwa na kikosi cha Great Britain kwenye michuano ya kimataifa ya jumuiya ya Ulaya mwaka 2016 na 2018.

Nyota huyo amefungiwa kujihusisha na mchezo huo wa riadha kuanzia usiku wa kuamkia leo baada ya vipimo kuonesha Chijindu alitumia dawa zisizopigwa marafuku michezoni kwenye michuano ya Olympic iliyofanyika Tokyo nchini Japan mwezi uliopita.

Taarifa zinaeleza kuwa, Chijindu amekutwa na vimelea vya Ostraine na S -23 kwenye mwili wake ambazo zinasisimia misuli na kumfanya achachuke na kutimua mbio zaidi licha ya njemba huyo mwenye miaka 27 yeye na timu yake ya Great Britain kushika nafasi ya pili na kupata medali ya fedha. Adhabu yaweza kuwa kubwa mpaka kupelekea timu yake kupoteza nafasi ya ushindi wa pili.

1 - Ni idadi ya siku iliyopita tokea Lionel Messi atambulishwe rasmi kuwa mchezaji mpya wa PSG ya Ufaransa akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na iliyokuwa timu yake, klabu ya Barcelona ya Hispania.

Rekodi zinaonesha kuwa tokea Messi atue PSG ndani ya hiyo siku moja, akaunti za mitandao ya kijamii ya klabu hiyo na mauzo ya jezi yamefanya kufuru kwani kabla Messi hajatua PSG, akaunti yao ya Instagram ilikuwa na wafuasi milioni 19.8 lakini mpaka kufika hii leo wamefika milioni 45.8, wafuasi milioni 25.8 wameongezeka zaidi. Kwa upande wa twitter inaelezwa wafuasi zaidi ya elfu 15 wameongezeka huku jezi 250,000 zilizochapishwa awali zimeripotiwa kumalizika huku jezi moja ikiwa na thamani ya euro 115 sawa na 313,000 za kitanzania, hivyo PSG inakadiriwa wameuza jezi hizo 250,000 ndani ya siku moja kwa euro milioni 28,750,000 sawa na bilioni 78 na zaidi ya milioni 239 za kitanzania.