Jumapili , 11th Jun , 2017

Tanzania usiku wa jana ilianza vibaya mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon baada ya kukubali sare ya 1-1 dhidi ya Lesotho katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mbwana Samatta akipiga shuti pembeni ya Thapelo Mokhele (kulia)

Katika mchezo huo Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa Nahodha wake, Mbwana Samatta kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki wa kushoto, Gardiel Michael kuangushwa nje ya boksi. 
Hata hivyo, bao hilo halikudumu, kwani Lesotho walisawazisha dakika ya 34 kupitia kwa Thapelo Tale aliyeunganisha pasi nzuri ya Jane Thaba-Ntso.
Kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini Lesotho ndiyo waliocheza vizuri  na kutawala mchezo sehemu ya kiungo.
Lesotho ilipata pigo dakika ya 40 baada ya mfungaji wa bao lake, Tale kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo hivyo kocha Moses Maliehea akamuingiza Motebang Sera.
Kasi ya mashambulizi ya Stars iliongezeka mwishoni mwa mchezo baada ya mabadiliko yaliyofanywa mfululizo na Mayanga akiwatoa Thomas Ulimwengu, Simon Msuva na Muzamil Yassin na kuwaingiza Farid Mussa, Mbaraka Yussuf na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Nahodha Samatta hakucheza vizuri kipindi cha pili kutokana na kuonekana kukerwa na namna wachezaji wa Lesotho walivyokuwa wakimdhibiti watatu kwa mkupuo.   


Simon Msuva akipiga mpira mbele ya mabeki wa Lesotho.
 

KIKOSI: TANZANIA
Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Farid Mussa dk71, Muzamil Yassin/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk71, Thomas Ulimwengu, Mbwana/Mbaraka Yussuf dk78, Samatta na Shiza Kichuya.

KIKOSI: LESOTHO
Likano Mphuti, Mafa Moremoholo, Bokang Sello, Kopano Seka, Thapelo Mokhelo, Bokang Mothoana, Tumelo Khutlang/Mabuti Potloane dk61, Tsoanelo Koetle, Taphelo Talle, Hlompho Kaleko na Jane Thaba Ntso.