Jumanne , 16th Nov , 2021

Mshambuliaji wa AS Roma, Tammy Abraham, amefunguka kuwa, siri ya yeye kukuwa kisoka kwa sasa inatokana na umahiri wa mafundisho ya kocha wake wa sasa Jose Mourinho anavyomuelekeza namna ya kukabiliana na mabeki wa timu pinzani.

(Mshambuliaji wa AS Roma, Tammy Abraham)

Nyota huyo ambaye alianzia maisha yake ya soka kwenye kituo cha kuvumbua na kukuza vipaji cha Chelsea 'Chelsea Academy' hadi alipopandishwa timu ya wakubwa na baada ya kutokupata nafasi ya kucheza mara kwa mara akapelekwa kwa mkopo kwenda klabu za Bristol City, Swansea City, Aston Villa na kurudi tena Stamford Bridge kabla ya kuuzwa kwenda Roma mwishoni mwa msimu uliopita wa mwaka 2020-21.

Alipoulizwa ni kwa kiasi gani Mourinho amemsaidia, alijibu ni, “kuwa mnyama kweli”, nafikiria kitu kimoja alichoniambia, nilikuwa laini laini na nahitaji kuwa mtu wa nguvu kama mshambuliaji.”

“Si suala la kuwa laini kwenye uwanja, unahitaji kuwa mtu wa nguvu, ili uwepo wako uwaogopeshe mabeki, nadhani hicho ndicho nilichojifunza na naendelea kukifanyia kazi,” aliongezea Abraham.

Abraham alijumuishwa tena kwenye kikosi cha England kilichocheza na Albania pamoja na San Marino katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Alisajiliwa Roma akitokea Chelsea kwa ada ya pauni milioni 34 na kusaini mkataba wa miaka mitano, huku pia kukiwa na kipengele cha Chelsea kuweza kumnunua tena kwa kiasi cha pauni milioni 68, lakini lazima awe amecheza misimu miwili.