Alhamisi , 6th Feb , 2020

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Februari  03, 2020 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi mbalimbali.

Waamuzi

Mwamuzi msaidizi namba mbili Kassim Safisha amefungiwa miaka mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea katika mechi namba 150: (Simba SC 3-2 Namungo FC ), ambapo adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni namba 39(1)(a) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

Katika mechi namba 157: (Azam FC 1-1 Mtibwa FC) mwamuzi Meshack Suda ameandikiwa barua ya kukumbushwa kufanya majukumu yake kwa umakini zaidi katika mechi iliyochezwa  Januari 30, 2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kamishina Abdallah Zongo ameondolewa kwenye orodha ya Makamishina kwa kosa la kutoa taarifa yenye mapungufu. Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia Kanuni namba 40(1) kuhusu Udhibiti Kamishina.

Aidha katika hatua nyingine Kamati hiyo imemepeleka kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kiongozi wa Friends Rangers, Heri Chibakasa ) kwa kosa la kupigana na washabiki wa timu pinzani katika mchezo wa Friends Rangers 0-1 Dodoma FC.

Pia Mwamuzi Salum Mkole amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kuonyesha udhaifu katika usahihi wa kutoa kadi katika mechi namba 29A: (Dar City Fc 1-0 African Sports) iliyochezwa Januari 31,2020 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 39(1) kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.