Jumanne , 8th Dec , 2020

Mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Gwambina, Mwinyi Zahera amesema vijana wake walicheza vyema katika mchezo dhidi ya Azam ingawa amekiri kuwa walicheza kwa kujihami katika kipindi cha kwanza .

Mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Gwambina, Mwinyi Zahera akizungumza na Waandishi wa Habari.

Zahera ambaye aliwahi kuifundisha Yanga, amesema vijana wake walionyesha nidhamu dhidi ya Azam hususan kipindi cha kwanza, lakini baada ya kubaini wapinzani wao walikuwa na mapungufu walifunguka kipindi cha pili ingawa bahati haikuwa upande wao na mchezo ukamalizika kwa suluhu.

''Ni kweli tulijihami kipindi cha kwanza, kwakuwa tulitambua ubora wa mchezaji mmoja mmoja na uzoefu wa Azam katika ligi, ingawa baada ya kuona hawakuwa sawa, kipindi cha pili tulisukuma sana mashambulizi kwao, haikuwa bahati kwetu lakini vijana wetu walikuwa hatari zaidi wakashindwa kufunga mabao'' alisema Zahera.

Suluhu ya jana imewafanya Gwambina iendeleze mwenendo mzuri katika mechi nne za mwisho ambazo wameshinda mbili na sare mbili ikiwemo dhidi ya vigogo Yanga na Azam Fc.

Gwambina ambao ni wageni katika ligi, wamefikisha alama 17 katika michezo 13, wakishikilia nafasi ya 10 ya msimamo wa VPL anatarajiwa kuivaa Dodoma jiji katika raundi ya 14.