Jumanne , 29th Aug , 2017

Mchezaji wa timu ya Mchenga BBall Stars, Amini Mkosa amesema mechi ijayo ya 'game 5' za fainali za Sprite BBall Kings haitaweza kuwa rahisi kwa madai wapinzani wao TMT watakuja kwa kasi na nguvu zaidi ili waweze kujitetea kupata ushindi siku hiyo.

Mchezaji wa timu ya Mchenga BBall Stars, Amini Mkosa.

Mkosa amebainisha hayo baada ya timu yake kuchezea kichapo kutoka kwa TMT kwa pointi 80-79 katika mchezo wa nne fainali za Sprite BBall Kings uliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

"Mechi ijayo ya 'Game 5' haitakuwa rahisi ila tumejipanga vizuri hasa 'mentaly' kwa sababu tunajua wapinzani wetu watakuja kwa nguvu zaidi ili waweze kujihami washinde mchezo huo", alisema Mkosa.

Pamoja na hayo Mkosa ameendelea kwa kusema "tunajua tulipokosea 'last game so' tumerekebisha makosa yetu lakini pia tulikuwa na wachezaji wenzetu wawili ambao walikuwa majeruhi  ila sasa hivi wamerejea katika hali nzuri. Tuko tayari kwa mchezo wa mwisho kwa sababu hii mechi ndiyo 'final' maana zilizopita zilikuwa kama tunasherehesha ila hapa yoyote anaweza kuwa bingwa".

"Tuwatoe hofu mashabiki zetu kuwa hiyo 'game' inayofuata inshaallah tutafanya vizuri na kuondoka na ubingwa. Tunajua kama wao wameumia zaidi kwenye 'games' tulizopoteza, ila isiwafanye wakate tamaa  kutushangilia, tunawaomba wajitokeze kwa wingi kuja kui-support timu yao, nasi tutapambana kwa ajili yao kuhakikisha tunachukua huu ubingwa", alisisitiza Mkosa.

Mechi ya mwisho ya fainali za Sprite BBall Kings 'game 5' kati ya TMT na Mchenga BBall Stars inatarajia kuchezwa Septemba 2 mwaka huu katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam.