Tuzo ya Mkwasa ya kocha bora VPL yazua mzozo

Jumatano , 8th Jan , 2020

Jana Januari 7, 2020 Shirikisho la Soka Tanzania TFF limetoa tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwezi Disemba pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa mwezi kwa mwezi huo.

Kocha bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi Disemba, Charles Mkwasa.

Tuzo ya mchezaji bora imekwenda kwa kiungo wa klabu ya Simba, Francis Kahata akiwashinda Hassan Dilunga wa Simba na Bakari Mwanyeto wa Coastal Union alioingia nao fainali, huku tuzo ya kocha bora wa VPL kwa mwezi Disemba ikienda kwa kocha wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, akiwashinda Juma Mgunda wa Coastal Union na Sven Vandenbroeck wa Simba.

Kipengele cha kocha bora wa mwezi kimeonekana kuzua sintofahamu baada ya kulalamikiwa na wadau wengi wa soka, ambao wanasema kuwa kocha Mkwasa hakustahili kushinda tuzo hiyo mbele ya kocha wa Simba na Coastal Union ambao walifanya vizuri zaidi yake kwenye mwezi huo.

Yanga imecheza mechi tatu mwezi Disemba, ikishinda mechi mbili ambazo ni dhidi ya Tanzania Prisons (1-0) na Biashara United (1-0) huku ikitoa sare na Mbeya City, Simba pia ikicheza mechi tatu na kufanikiwa kushinda mechi zote tatu ambazo ni dhidi ya Ndanda FC (2-0), KMC (2-0) na Lipuli FC (4-0).

Coastal Union nayo imecheza mechi tatu mwezi Disemba, ikishinda mechi zote tatu dhidi ya Mbeya City 1-0, Azam FC 1-0 na Tanzania Prisons 2-0.

Afisa habari wa Simba, Haji Manara ni mmoja ya ambao hawajaridhishwa na tuzo hiyo kupewa kocha Mkwasa, ambapo amesema, "Mkwasa hakustahili kushinda hii tuzo kwa mwezi Disemba, kacheza mechi tatu, Mbeya City 0-0, Prisons kashinda 1-0 na akashinda 1-0 dhidi ya Biashara. Kocha wa Simba naye kacheza mechi tatu zote kashinda tena kwa magoli mengi zaidi, 4-0 na Lipuli, 2-0 dhidi ya Ndanda na KMC lakini hata kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda kafanya vizuri kuliko Mkwasa".