Ijumaa , 24th Jun , 2016

Bondia bingwa wa uzito wa juu duniani Tyson Fury amejitoa kwenye pambano la kutetea mikanda yake ya dunia ya WBO, WBA na IBO uzito wa juu na Wladimir Klitschko mwezi ujao baada ya kuumia kifundo cha mguu.

Tyson Fury akiwa amepumzika akionyesha eneo la mguu lililoumia.

Bingwa huyo wa dunia aliyeumia wakati anafanya mazoezi ya kukimbia eneo la Lake District, ametangaza kuahirisha pambano hilo lililokuwa lifanyike Julai 9 Mjini Manchester, nchini Uingereza.

Fury amesema: "Kwa takribani siku 10 zilizopita nilikuwa ninakimbia Lake District na nikaangukia kifundo cha mguu na kuumia".

"Nimekwenda hospitali na kufanyiwa vipimo vya MRI na X-Rayf. Sijavunjika, lakini ni maumivu makubwa na nimeambiwa ni pumzike kwa wiki sita saba," alisema Fury na kuongeza "Nilijaribu kuendelea na mazoezi hivyo hivyo, ili kupata maoni mengine wiki moja baadaye, lakini ni ushauri ule ule, hivyo pambano litaahirishwa,".

Fury ameomba radhi kwa mashabiki wake ambao walitaraji kuona akiendeleza ubabe kwa nguli huyo wa masumbwi kutoka Ukraine na kuwapa furaha mashabiki hao ambao watapokea kwa mshtuko taarifa ya kufutwa kwa mpambano huo ambao ungekuwa ni zaidi ya kutetea mikanda ila ungekuwa wa nani zaidi na kisasi.

Fury anayejulikana kwa jina la utani 'The Gypsy King', alimaliza utawala wa zaidi ya muongo mzima wa Klitschko kama bingwa wa uzito wa juu wa ndondi za kulipwa duniani baada ya kumshinda kwa pointi ukumbi wa Esprit Arena mjini Dusseldorf, Ujerumani Novemba mwaka jana.