Jumatatu , 30th Jan , 2023

Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi, amekiri kufurahishwa na hatua ya kurejea mazoezini kwa Kiungo kutoka nchini Uganda Khalid Aucho.

Kwa muda wa siku kadhaa Aucho amekuwa nje ya kikosi cha Young Africans, ambacho kinaendelea na harakati za kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Kocha Nabi amesema, kiungo huyo tangu Jumamosi amekua akifanya mazoezi binafsi baada ya kupona majeraha yake, na anaamini kurejea kwake mazoezini kutaongeza changamoto kwa wachezaji wengine wa Young Africans.

“Nimefurahi kuona kikosi changu kikiwa imara kutokana na uwepo wa baadhi ya wachezaji ambao walikosekana katika michezo iliyopita kwa ajili ya majeraha.”

“Kati ya hao ni Aucho ambaye amepona majeraha yake yaliyomsababisha aikose michezo iliyopita.”amesema kocha Nabi.

Aucho ameanza mazoezi mepesi chini ya uangalizi wa madaktari wa Klabu ya Young Africans, ambao wanachukua tahadhari zote ili kiungo huyo asijitoneshe majeraha yaliyomuweka nje kwa muda wa siku kadhaa.