Jumamosi , 24th Jul , 2021

Kocha wa kikosi cha mabingwa wa Tanzania Bara na mabingwa watetetzi wa komba la Azam Sports Federation Cup Simba SC, Didier Gomes Da Roa, amesema kikosi chake kipo tayari kuikabili klabu ya Young Africans kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho kesho Jumapili Julai 25.

Kikosi cha Simba

Mapema leo Kocha Gomes akiwa kwenye mkutana na waandishi wa habari akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa fainali kesho dhidi ya Yanga  amesema,

“tunataka kumaliza msimu huu vizuri, tunataka kuwafurahisha mashabiki wetu lakini pia ni muhimu sana kushinda kombe hili ili iwe mara ya pili. Kesho tutakuwa na mchezo wa aina nyingine na nawaamini wachezaji wangu wanataka kushinda”.

Nahodha msaidizi wa Simba Mohamed Hussein nae alizungumza kwa upande wa wachezaji namna walivyojiandaa kueleka mchezo huo, akisisitiza wamejipanga kushinda kesho.

“Maandalizi yameenda vizuri na sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri. Tunajukumu kubwa sana kwa timu yetu na kufanya vizuri kesho ndio italeta taswira ya ukubwa wa Simba. Sisi kama wachezaji jukumu ni moja kuhakikisha kesho tunaondoka na matokeo mazuri”- Amesema Mohamed Hussein kwenye mkutano na wanahabari.

Mchezo huu wa fainali ya kombe la Azam Sports Federation kati ya Simba dhidi ya Yanga utachezwa katika dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma, mchezo utachezwa kuanzia Saa 10:00 Jioni. Na matangazo ya mchezo huu utayasikiliza moja kwa moja kupitia East Afrika Radio 88.1 Dar es salaam lakini pia kupitia mtandao www.eastafricaradio.com