Jumanne , 21st Jul , 2020

Uongozi wa klabu ya Simba sc kupitia kwa mtendaji mkuu wa timu hiyo Senzo Mazingisa umekanusha taarifa zinazoenea kuwa timu hiyo inampango wakuliondoa benchi zima la timu hiyo pamoja na wachezaji mbalimbali katika kipindi cha dirisha kubwa la usajili linalotarajia kuanza july 31 2020.

Makocha wa mabingwa wa VPL,Sven Vandenbroeck (kushoto) na Seleman Matola (Kulia) wakijadili jambo kabla ya mazoezi ya kikosi chao.

Akizungumza na East Africa Radio Senzo amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote na zina lengo la kuharibu dhamira ya klabu hiyo huku akisisitiza kuwa hakuna Mtu yoyote ayakayefukuzwa kwenye timu hiyo na makocha wao Sven Vandenbroeck na Seleman Matola wapo kwenye mipango yao.

Aidha Senzo ameweka wazi kuwa wamepokea ripoti kutoka kwa benchi la ufundi juu ya usajili na wataifanyia kazi ili kutekeleza matarajio yao ya msimu ujao katika ligi ya mabingwa barani afrika.
UVUMI UMETOKEA WAPI?

Siku moja baada ya klabu ya Simba kukabidhiwa taji lake la ligi kuu mkoani Lindi, viongozi wa timu hiyo waliratibu sherehe za mapokezi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu JK Nyerere.

 

Liliandaliwa gari la wazi, ambalo lilitakiwa kuwabeba wachezaji ambao wangelitembeza taji la VPL katika mitaa mbali mbali jijini Dar es salaam.

 

Wakati zoezi hilo likiwa limeandaliwa, kocha Sven alionekana kupinga utaratibu huo na kuwaamuru wachezaji wapande kwenye gari za kawaida ili waende kambini kujiwinda na mchezo wa dabi baina yao dhidi ya Yanga ikiwa ni nusu fainali ya kombe la FA ambao walishinda kwa bao 4-1.

Kitendo cha kocha huyo kugomea shughuli ya kulitembeza kombe, kilitajwa kuwa kimetafsiriwa kama ni jeuri na asiye shaurika.

Pia ukiacha na hilo, inatajwa kwamba kocha huyo hana mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzake katika benchi la ufundi, na inadaiwa ni mtu asiyeshaurika.

KIPI KINAHUSISHWA ZAIDI NA MABADILIKO YA BENCHI LA UFUNDI?

Jambo jingine linalohusishwa na kuvunjwa kwa benchi zima la ufundi la Simba ni kutokana na matamanio ya wekundu hao kufanya vyema katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika.

Klabu hiyo imekua ikihusishwa na kocha wa AS Vita ya DR Congo, Florent Ibenge ambaye ana uzoefu mkubwa wa michuano hiyo akiwa na wababe hao wa Congo.

Simba iliyokua ikinolewa na Patrick Aussems ilicheza hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika lakini ilitolewa na TP Mazembe msimu juzi lakini ilishindwa kufurukuta katika msimu uliopita baada ya kutupwa nje kwenye hatua za awali na UD Songo ya Msumbiji .