Jumatatu , 20th Nov , 2023

Timu ya Red Bull ya mchezo wa kukimbiza magari Langa langa (Formula 1) imeweka rekodi mpya ya kushinda mbio 20 ndani ya msimu mmoja na kuvunja rekodi ya Mercedes Benz ya mwaka 2016 ambao walishinda mbio 19 kati ya 21 kwenye kalenda ya F1 ya mwaka huo.

Max Verstappen dereva wa Red kulia akiwa na kiongozi msimamizi wa timu hiyo Christian Horner wa kushoto.

Baada ya Dereva wa Red Max Versatappen kushinda mbio za Las Vegas GP jana Jumapili Novemba 19 ameifanya timu hiyo kuwa imeshinda mbio 20 kati ya 21 zilizofanyika mpaka sasa msimu huu wa 2023 ambao una mbio 22. Zikiwa ni mbio nyingi zaidi kwa timu moja kushinda kwenye kalenda ya mwaka wakiwa na wastani wa 95.2% za ushindi.

Zikiwa zimesalia mbio za Abu Dhabi kufanyika kabla ya kukamilisha kalenda ya F1 kwa mwaka 2023, Red Bull imeweka rekodi ya kukusanya alama nyingi zaidi kwenye historia ya Langa langa wana alama 822 na wanaweza kufikisha alama 866 kama wakishinda mbio za Abu Dhabi zitakazofanyika Novemba 26.

Kwenye mbio hizo 20 walizoshinda mbio 18 ameshinda Max Verstappen ambayo ni rekodi kwa dereva kushinda mbio nyingi kwa ndani ya msimu mmoja, mbio nyingine mbili ameshinda Sergio Perez. Dreva pekee nje ya Red Bull aliyeshinda Grand Prix msimu huu ni Carlos Sainz wa Ferrari.