Jumatano , 27th Mei , 2020

Klabu za Simba na Yanga ziko katika vita ya kuwania saini ya mlinzi matata wa klabu ya Coastal Union, Bakari Nondo Mwamnyeto kuelekea msimu ujao wa 2020/21.

Haruna Niyonzima wa Yanga, Luis Miquissone na Meddie Kagere wa Simba

Beki huyo amekuwa katika midomo ya wadau wengi wa soka msimu huu kutokana na umahiri wake wa kuzuia na kuisaidia klabu ya Coastal Union kufikia katika nafasi nzuri msimu huu.

Wakala wa mchezaji huyo ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa soka katika mkoa wa Tanga, Kasa Mussa amethibitisha mchezaji huyo kuhitajika na klabu hizo kubwa nchini na kwamba kinachosubiriwa ni msimu kumalizika ili waweze kukamilisha dili na moja ya klabu hizo.

Amesema kuwa Yanga wameonesha nia ya kumuhitaji pamoja na Simba lakini mpaka sasa hajafikia makubaliano ya dau la uhamisho na klabu ya Yanga ambao ndio wako katika mazungumzo mazuri.

Klabu ya Yanga imesharejea mazoezini jana baada ya kukamilisha vipimo vya wachezaji na benchi la ufundi, hivyo leo mazoezi rasmi yanatarajia kuanza sambamba na Simba na Azam FC ambao wanatarajia pia kuanza mazoezi yao leo.

Pia Serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania BMT inatarajia kutoa mwongozo rasmi kuelekea kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza na la Pili, ikiwemo suala la mwongozo wa afya.