Jumatatu , 23rd Jul , 2018

Droo ya mechi za nusu fainali ya Sprite Bball Kings imefanyika usiku  wa Julai 23, kwenye ofisi za East Africa Television na kurushwa moja kwa moja kupitia kipindi cha '5Sports' na kusikika kupitia 'The Cruise' ambapo mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars watakutana na Portland.

Manahodha wa timu 4 zilizopo hatua ya nusu fainali.

Katika mechi hiyo timu ya Portland itakuwa ndio timu mwenyeji kwenye nusu fainali ambayo itakuwa na jumla ya mechi tatu 'Best of three' lakini ikitokea timu moja imeshinda mechi mbili mfululizo, inakuwa imetinga fainali moja kwa moja hivyo mechi ya tatu haitakuwepo. Endapo kila timu itashinda mechi moja kati ya hizo mbili italazimika kuchezwa mechi ya tatu ili kuamua nani anakwenda fainali.

Droo hiyo pia imezikutanisha timu za Flying Dribblers ambao watakuwa wenyeji wa Team Kiza kwenye nusu fainali nyingine ambayo nayo itachezwa kwa mtindo huo huo wa mechi tatu ambazo zitafikiwa endapo timu hizo zitagawana ushindi kwenye mechi mbili za kwanza.

Mechi hizo za kwanza kwenye nusu fainali hiyo zitapigwa Jumamosi Julai 28, 2018 na mechi za pili zitapigwa Jumatano Agosti 1. Viwanja ambavyo vitatumika vitatangazwa hivi karibuni endelea kukaa karibu na East Africa Television na East Africa Radio.

Katika mechi za robo fainali Mchenga walishinda pointi 84 dhidi ya 67 za St. Joseph huku Portland wakiitoa Temeke Heroes kwa vikapu 84 dhidi ya 70. Flying Dribblers wao waliwatoa Water Institute kwa pointi 100 dhidi ya 64. Team Kiza waliiadhibu DMI kwa pointi 82 kwa 47.

Bingwa wa mashindano haya yanayodhaminiwa na kinywaji baridi cha Sprite, atajinyakulia kitita cha shilingi milioni 10 huku mshindi wa pili akitwaa milioni 3 na mchezaji bora wa mashindano 'MVP' akiondoka na shilingi milioni 2.