Waamuzi wapo tayari kutenda haki

Jumanne , 7th Aug , 2018

Kuelekea mchezo wa kesho Jumatano Agosti 11 wa game 3 ya 'best of three' nusu fainali ya michuano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings kati ya Portland dhidi ya Mchenga Bball Stars, Kamishna wa ufundi wa TBF Manase Zabroni amesema waamuzi wamejipanga kuhakikisha haki inatendeka.

Waamuzi wa Kikapu wakiongozwa na Manase Zabroni (kulia).

''Kama tulivyoanza mwanzo wa mashindano kumekuwa hakuna lawama kuhusu waamuzi hivyo tutamaliza nusu fainali kesho kwa mwendo huo na mshindi atapatikana kwa haki na atakwenda kucheza fainali na wenzao wa Flying Dribblers ambao nao wamefika hatua hiyo bila malalamiko kwa waamuzi'' - amesema.

Mchezo wa kesho utazikutanisha timu za Portland dhidi ya Mabingwa watetezi wa michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji cha Sprite, Mchenga Bball Stars. Mchezo huo ambao umekuja baada ya timu hizo kushinda mechi moja kila timu kwenye game 1 na game 2, utapigwa kwenye viwanja Don Bosco Oysterbay.

Mchenga Bball Stars (nyeupe) na Portland (kijani) kweye mechi ya game 2.

Portland walitoka nyuma kwa kupoteza game 1 kwa pointi 70 kwa 54 kabla ya kusawazisha game 2 kwa kushinda pointi 71 kwa 64. Game 3 itakuwa na ushindani mkubwa hususani kwa vinara wa pointi katika timu hiyo ambao ni Denis Babu kwa Portland mwenye pointi 104 kwenye mechi 5 na Baraka Sadick wa Mchenga mwenye pointi 64 katika mechi 4.

Mechi hiyo itakayotoa tiketi ya kwenda kucheza fainali na Flying Dribblers kuwania milioni 10 kwa bingwa, milioni 3 kwa timu itakayoshika nafasi ya pili na milioni 2 kwa MVP itaanza majira ya saa 10:00 jioni.